Sunday, March 11, 2012

JUMAPILI YA 3 YA KWARESMA 11/03/2012

Masomo: I. Kutoka 20:1-17

              II. 1Kor 1:22-25

            III. Yohane 2:13-25

Tafakari:
            Katika kutafakari Kwaresma, tunaalikwa na somo la kwanza kuzitafakari Amri za Mungu. Mungu anawakumbusha Waisraeli kuwa ndiye aliyewatoa utumwani, ana agano nao na hivyo anawapa amri za kuzingatia katika agano hilo.
            Maelezo ya amri hizo yameelezwa vizuri katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Kwa ufupi amri hizi ni za kutuongoza ili kuhusiana vema na Mungu na ndugu zetu ambazo Kristu anatoa ufupisho wake katika amri kuu mbili; Kumpenda Bwana Mungu kwa Moyo wote, akili na nguvu zote. Pia kumpenda jirani kama nafsi zetu.Sheria/amri ni kwaajili ya kurahisisha maisha na si kwa lengo la kumuadhibu yeyote!  
            Somo la Injili tunaona kuwa kwasababu ya kutoziheshimu amri na taratibu, Yesu anaingilia kati na kupindua meza zao.
            Anaposema “Libomoeni hekalu hili na kwa siku tatu nitalisimamisha” anatabiri juu ya kifo na ufufuko wake. Hekalu ni mwili wake! Mtume Paulo katika waraka wake wa kwanza anaonesha kuwa kama wakristu tunashiriki katika fumbo hilo kwa kuwa sisi nasi ni hekalu la Roho Mtakatifu.
            Ikiwa basi sisi ni mahekalu ya Mungu, hatuna budi tufungue mioyo ili Kristu atusafishe na kila udhalimu na kila aina ya biashara ifanyikayo ndani yake, yaani , yale mambo yote yaliyo kinyume na mapenzi ya Mungu.
            Tuwakumbuke, siku ya leo, wakatekumeni wanaofanyiwa leo takaso la kwanza!

No comments:

Post a Comment