Friday, March 9, 2012

JUMAPILI YA 2 YA KWARESMA 04/03/2012


Masomo: I. Mwanzo 22:1-2, 9a, 10-13,15-18
               II. Rum 8:31b-34
              III. Mk 9:2-9
Mhubiri alisema:
            Changamoto ya siku ya leo ipo katika somo la kwanza, ambapo japo Ibrahimu alikuwa ana mtoto mmoja tu aliyempata kwa Sara katika uzee… tujiulize, Angemchinja Isaka, ahadi ya uzao mkubwa angeitimizaje? Hata hivyo Ibrahimu hakusita kumtoa Isaka-mwanae wa pekee sadaka kwa Mungu akiamini kuwa, yeye aliyempatia mwana katika uzee, atajua ni kwa jinsi gani atampatia huo uzao mkubwa kama mchanga wa pwani. Kutokana na tendo hili la ushujaa, Ibrahimu anastahili kuwa Baba wa Imani!
            Kumtolea Isaka (katika agano la kale) ni kielelezo cha Mungu alivyomtolea mwanae wa pekee – Yesu Kristu (katika agano jipya) kwaajili yetu!
            Katika somo la III – Injili, tukio la kung’ara sura kwake Yesu linatanguliwa na matukio kadhaa: - Yesu alimponya kipofu hatua kwa hatua (Mk 8:22-26) ikiwa ni ishara ya kuwafunua macho wafuasi wake juu ya utume wake wa kimasiha hapa duniani; kisha anawauliza kuona kama wamtambua yeye ni nani (Mk 8:27…)
            Kumbe tukio hili la kung’ara sura ni mwendelezo wa mafundisho ya Yesu kwa wafuasi wake juu ya kumtambua yeye ni nani na utume wake ni upi hapa duniani. Turejee katika Injili hii na tutafakari juu ya mambo yafuatayo yanakutwa humo:
Ø      Mlima mrefu
Ø      Kung’ara  ni dhihirisho la utukufu wa Kristu
Ø      Eliya ni mwamba mmojawapo wa agano la kale. Huyu ni nabii mkuu aliyepambana na dini za kipagani na kuzishinda. Anatabiriwa kuwa atarudi kumtayarishia masiha njia kwa vile hakufa bali alitwaliwa. Uwepo wake katika tukio hili waonesha ujio wa masiha.
Ø      Musa ni mwamba mmojawapo wa agano la kale. Huyu naye ni nabii mkuu – mtoa Torati, aliyewahi kuongea na Mungu uso kwa uso ambaye aliwaahidi waisraeli kuwa yuaja nabii mkuu kama yeye atokaye kwa Mungu – ndiye Kristu (Kumbukumbu la Torati 18:15)
Ø      Sauti yadhihirisha kuwa Kristu ni nabii mkuu
Ø      Wingu laashiria uwepo wa Mungu na kuhakiki utume wa Kristu-Masiha (Kutoka 19:9, 13:21, 33:9-11)
Ø      Vibanda ni rejeo la sikukuu ya vibanda (Zekaria 14:16-19) kuashiria kumbukumbu ya kukaa kwa waisraeli jangwani na tarajio la masiha. Sherehe hii ilitabiriwa kuendelea kuwepo hata baada ya ujio wa masiha.
Ø      Hofu  ni namna ya msisimko wa furaha na woga. Uwepo wa Bwana ni sharti uambatane na furaha yenye mshangao pamoja na tetemeko (Tremendum Fascinantia)
Tujifunze nini kutokana na haya:
-         Kuwa na ushujaa wa Imani kama babu yetu Ibrahimu tukimtumainia Mungu katika kila jambo.
-         Kuachana na malimwengu ili tuambatane na Kristu huku tukiikumbata imani kwake.
-         Tuache maisha mabovu ya dhambi ili tuifikie furaha na amani ya kweli.
Tujiulize pia:
Mambo yakienda kinyume cha matarajio yetu, je, twaweka tumaini na imani kwa Mungu?
            Mtume Paulo katika somo la II, anasema: Ni nani awezaye kututenga na Kristu kama tumeshikamana naye? Hata kama tutaonekana kama tumeachwa naye, tusimame imara, tusikate tama kwani mateso, kifo ni lazima ili kuufikia utukufu. Tukumbuke kuwa:
-         Hakuna Pasaka bila Ijumaa kuu,
-         Mchumia juani hulia kivulini,
-         Subira huvuta heri,
-         Mvumilivu hula mbivu; na
-         Mtaka cha uvunguni sharti ainame.

No comments:

Post a Comment