Karibuni
tutafakari pamoja kipindi cha kwaresma ni mwafaka kwa tafakari kama hii. Yesu anapotuambia tubuni na kuiamini injili
(rej. Mk 1:15) anasisitiza kutubu dhambi siyo “kubuni dhambi.” Tunatambua wazi
kuwa kuna watu kati yetu wanaobuni dhambi daima iwe kipindi cha kwaresma au la.
Kuna watu wanabuni namna ya kubomoa nyumba za watu au mabenki (majambazi). Kuna
watu wanabuni mbinu mpya za kikahaba (makahaba). Kuna watu wanabuni mbinu za
rushwa (mafisadi). Watu wengine wanabuni namna ya kuwaudhi wenzao ili wao
wafurahi (sophists). Wengine wanabuni bomu la kulipua ubalozi (magaidi) na
mambo mengine mengi. Tuombeane sote hasa kipindi hiki cha kwaresma.
Kusema kweli
haya ndiyo baadhi mambo ambayo Yesu anatufundisha kuyaacha. Hii ndiyo kazi yake
kubwa na ya kwanza. Tukitafakari masomo ya jumapili kama tatu hivi kabla ya
jumapili ya kwanza ya kwaresma tutaelewa vizuri sana . Tunaona kuwa Mama Kanisa anatuanda
vizuri kuupokea ujumbe wa kutubu na kuiamini injili. Yesu anatenda miujiza
mingi ilimradi tu watu watubu na kuiamini injili. Kimsingi miujiza ilikuwa ni
namna ya kuelezea lengo lake (by the way). “ ‘Watu wote wanakutafuta’
akawaambia ‘twendeni mahali pengine katika vijjiji vya jirani nipate kuhubiri
huko pia.’ Hiyo ndiyo nia ua kuja kwagu.” (Mk 1:38). Mtume Paulo naye
anasisitiza “ole wangu nisipoihubiri injili”(1Kor 9:16). Kuiamini na kuiishi
injili ndiyo njia pekee ya kutuepusha kuwa wabunifu katika dhambi, kuondolewa
pepo na kupewa mikate haitoshi.
Kipindi hiki cha
kwaresma tusibuni dhambi badala yake tuwe “wabunifu katika kuungama dhambi”
yaani; kumwomba Roho Mtakatifu, kutafuta dhambi moyoni, kujuta dhambi,
kukusudia kuacha dhambi, kuungama dhambi, kupokea maondoleo ya dhambi na
kutimiza malipizi. Habari ya mwana mpotevu inatutafakarisha hatua hizi za
wongofu (metanoia - Rej. Lk 15:11-32). Tuwe wabunifu ndani ya
nafsi zetu wenyewe tukijiuliza mbona nikiudhiwa kidogo tu napata
hasira kali sana ,
moyo unajaa gesi inayoweza kuua? Tukumbuke kuwa kuna mahusiano kati ya dhambi
na maisha ya udhalimu. Kadiri mtu anavyokuwa mbunifu katika dhambi ndivo
anavyokuwa mtumwa wa mambo mengi mabaya yanayomuasili yeye na jamii (Rej Dan
9:3-20; Ezr 9:6-15; Mt 3:7-9; Rum 6:23). Maana ya kukusudia kuacha dhambi ni
kuazimia kuacha dhambi na kuepa nafasi zake (Rej Mt 5:29-30).
Tumwombe Mungu
mwenye huruma ili kwaresma hii tuitikie vyema mwaliko wa Papa Leo Mkuu katika
mahubiri yake kipindi cha Krismasi akisisitiza; “Ewe mkristu, tambua cheo chako
umeshirikishwa hali yake Mungu mwenyewe kwa hiyo usianguke tena katika fedheha
na ubovu wa maisha yako ya kale…” (Sala
ya Kanisa uk.94)
Tumsifu Yesu
Kristu!
Na. Frt Hillary Faraja - Theology III - (Geita Diocese)
No comments:
Post a Comment