Wednesday, February 22, 2012

KANISA NI MOJA KWA SABABU YA ROHO MTAKATIFU:


Roho Mtakatifu yuko katika Kanisa na neema zake zote. Mt.Ambrose asema kwamba, Kanisa lilijengwa na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu  ndiye anaunganisha viungo vyote vya Kanisa vilivyo mwili wa Kristo na Kuleta umoja. Hili tendo la kuunganisha kanisa laendelea kukua na kuhusisha kila mmoja. Hivyo, Kanisa likihusisha kila mmoja ,litaendelea kukua kupitia kwa Neno, Sakramenti, vipaji na huduma mbalimbali, lakini hasa kwa upendo.Tutafahamu zaidi huu uhusiano tukirejea maelezo ya Kanisa katika imani tunayosadiki.
Roho anayeishi kwa kila Mkristo ndiye anayewafanya waunganike kikamilifu katika kristo.Hiyo ndiyo maana ya kuwa .Sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika huo mwili mmoja (1kor1:2, 13; Efe 4:4).
Kanisa kama alivyoeleza Mt.Sipriano “ni watu waliokusanyika katika umoja, Baba, Mwana na Roho” Roho Mtakatifu ndiye nguzo ya umoja wa Baba anayeunganisha wote katika Kanisa waliobatizwa katika mwili mmoja, yaani mwili wa Kristo. Roho Mtakatifu ni mmoja asiyegawanyika na hivyo huleta wote pamoja na kuwafanya kuonekana kama kitu kimoja ndani yake.
Roho Mtakatifu anaunganisha kwa maana upendo huunganisha.Twasoma ya kwamba, “Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho aliyetupatia. Roho Mtakatifu ndiye mwimarishaji wa umoja siyo tu kati ya watu binafsi na wengine, bali pia kati ya Kanisa binafsi na lile Kanisa moja pekee” (CCC879).
Hapa ushirika wa Kanisa kama ulivyoanzishwa na mitume kumi na wawili waliounganika na Kristo chini ya uongozi wa Petro,unadhihirika wazi (LG 19)
Kila Kanisa mahalia ambalo ni sehemu ya watu wa Mungu inapata kutambulika ikiwa na Baba Mtakatifu  aliye mtumishi wa cheo cha Petro pamoja na Baraza la Maaskofu nchini kwa nguvu ya Ekaristi Takatifu. Kila Kanisa binafsi ni Kanisa moja zima likishirikiana na mengine yenye kuungama Ekaristi moja.
Roho Mtakatifu yupo katikati ya muungano kamili wa Kanisa. Katika Mtaguso wa Pili wa Vatikani, Kanisa lilitangaza kwamba makanisa yasio ya kikatoliki na jumuiya za wakristo wa Kanisa Katoliki zimeunganishwa ndani ya Roho Mtakatifu kwa vipaji na neema za Roho Mtakatifu. Kwa nguvu za utakasaji amewaimarisha wengi wao hata kufikia kumwaga damu.
Hivyo Roho Mtakatifu huleta umoja wa Kanisa  na pia mgawanyiko ( sio utengano) kwa kuwapa waumini vipaji mbali mbali na Makanisa binafsi
imeandaliwa na:
Frt BikolwaMungu A, Stephen (Jimbo kuu la Mwanza)

No comments:

Post a Comment